Total Pageviews

Friday, 27 January 2017

UHAKIKI WA RIWAYA YA JOKA LA MDIMU YA ABDALAH SAFARI


Imeandaliwa na Livin Kimario
 
JOKA LA MDIMU

 

MAUDHUI

A;DHAMIRA

1.      HALI NGUMU YA MAISHA

Riwaya mezungumzia ugumu wa maisha kwa wananchi unaosababishwa na hali mbaya ya uchumi wa nchi. Masikini ndio wanaothirika sana hawana uwezo wa kujikimu katika maisha yao ya kila siku wanaishia kufanya kazi za kijungujiko tu. Kuumia huku kwa watu wa kawaida kunasababishwa na siasa na uongozi mbaya,uhaba wa mafuta,mfumuko wa bei,rushwa, magendo,ufisadi na kutowajibika kwa viongozi. Kwa mfano uhaba wa mafuta umesababisha tatizo kubwa la usafiri na watu kukosa mwanga usiku majumbani.(uk 01)

Pia ugumu wa maishaunawafanya watu kukosa chakula na kula mahindi ya njano(uk. 15-16).

Pia ugumu wa maisha unawafanya wananchi kufanya kazi ngumu na kutochagua kazi za kufanya ilimradi mkono uende kinywani(uk. 46-50) mhusika Jinja Maloni anaonekana akifanya kazi ya kuchimba makaburi na kuapkua vyoo kwa namna ambayo si rahisi wengi kuifanya.

Hali ngumu ya maisha inafanya wakulima waache kulima mazao ya bishara kwani kilimo kimeonekana kutoasaidia kabisa(uk. 39-40)

Pia mwandishi ameonesha kuwa ugumu wa maisha unaneshwa na ubovu wa barabara na huduma nyingine za kijamii na kiafya,watu  kuwa na makazi na mavazi duni.

 

2.      RUSHWA

Mwandishi ameonesha kuwa rushwa ni kichocheo cha ugumu wa maisha na imeenena katika karibu kila sekta,watu wanalazimika kuhonga ili kupata huduma ambazo ni haki yao.

Mfano; mwandishi ameonesha jinsi mkewe Tino alivyopata shida kusafiri kwenda mjini mpaka walipotoa hongo.(uk 71).

Pia tumeoneshwa jinsi Amani alivyompa Dakta Mikwala rushwa ya vyakula,vinywaji na fedha ili aidhinishe Cheche akatibiwe Uingereza na hatimaye kibali kikatolewa.

Pia Brown Kwacha alipokea rushwa ili kutoa huduma kwa watu mbalimbali,kwani tumeoneshwa Shiraz Bhanj akimweleza kwamba amemwekea fedha katika akaunti yake ya Geneva na pia aliomba kiasi cha fedha kwa Amani ili aidhinishe fedha za Cheche kwenda kutibiwa nje ya nchi.

Pia Brown Kwacha alitoa rushwa ili apate viwanja alivyohitaji.Na akavipata kadiri ya alivyohitaji.

 

 

 

 

 

 

3.      URASIMU

Mwandishi ameonesha jinsi ukiritimba wa viongozi unavyoongeza ugumu wa maisha kwa wananchi na kukwamisha maendeleo. Mfano Cheche baada ya kuumia katika sherehe za uhuru alitakiwa kupelekwa nje kwa matibabu lakini sababu kadhaa zisizo na ukweli wowote kama vile serikali haina fedha za kigeni,kwanini wakaombe kibali bila ahadi n.k (uk. 138). Zilitolewa na wahusika na kufanya haki ya Cheche kadiri alivyostahili kukoekana.

Kunapokuwa na viongozi warasimu kama hawa ugumu wa maisha unakuwa maradufu.

 

4.      KUTOWAJIBIKA

Mwandishi anaonesha jinsi viongozi walio wengi wasivyotimiza wajibu wao kama inavyotakiwa katika ofisi za umma wanazozitumikia. Wanageuza ofisi hizo kama mali yao binafsi,sehemu ya kufanyia ufuska,biashara haramu,upendeleo nk. Mfano tumeona jinsi Brown Kwacha alivyoigeuza ofisi ya umma kama sehemu ya kufanyia ufuska,kupendelea katika utoaji wa huduma hasa kwa wanawake n.k (uk. 94).

 

5.      NAFASI YA MWANAMKE KATIKA JAMII

Mwandishi amemchora mwanamke katika nfasi mbalimbali kama ifuatavyo;

a)      Mwanamke ni mzazi na mlezi mzuri. Mfano ni Mwema mkewe Tino aliwalea viizuri sana watoto wake Cheche, Tabu na Subira pia alimpenda na kumtunza vyema mumewe. Pia mke wa Brown Kwacha aliwalea vyema mabinti zake watatu kwa kiasi kikubwa peke yake bila msaada wa karibu wa mumewe.

b)      Mwanamke ni chombo cha starehe,yaani chombo cha kuwastarehesha wanaume pindi wajisikiapo. Mfano tumeona jinsi wanaume mabaharia walivyokuwa wakiwatumia wanawake kujistarehesha,pia Brown Kwacha alikuwa na wanawake wengi ambao kikukweli hakuwapenda kwa dhati na aliwatumia kukidhi haja zake za kimapenzi.

c)      Mwanamke kama kiumbe duni asiyeweza kutoa mchango wowote wa mawazo, haya yanadhihirishwa na jinsi mkewe Brown Kwacha alivyokuwa hashirikishwi na mumewe katika jambo lolote mumewe alilofanya atoe mchango wake wa mawazo.

d)     Mwanamke kama mtu jasiri,mfano tumeona jinsi Pamela alivyokuwa na ujasiri na uthubutu pamoja msimamo wa kumkataa kimapenzi Br own Kwacha bila kujali hadhi na uwezo wake.

 

6.      MATABAKA

Mwandishi ameonesha kuwapo kwa matabaka mawili katika jamii,tabaka la wenye nacho/matajiri na wale wenye nafasi kiutawala pamoja na tabaka la masikini/watawaliwa. Tabaka la juu wanawakandamiza tabaka la chini kwa njia mbalimbali,tabaka la juu linawakilishwa na kina Bhanj,Brown Kwacha na viongozi wa serikali huku tabaka la chini wanawakilishwa na kina Tino,Jinja Maloni na Amani.

 

 

 

 

7.      USHIRIKINA

Mwandishi ameonesha kuwa bado wanajamii wengine wanaamini katika nguvu za giza katika kufanya mambo yao huku wakiwa na uwezo na nguvu za kawaida za kufanya mambo hayo. Mfano tumeoneshwa jinsi viongozi na wachezaji wa timu ya Sega Warriors walivyokwenda kwa Sangoma ili awasaidie washinde mechi yao dhidi ya City Devils.

 

 

8.      UHUJUMU UCHUMI NA MAGENDO

Mwandishi ameonesha jinsi viongozi na baadhi ya wananchi wanavyohujumu uchumi wa  nchi na wanayojihusisha na biashara za magendo na ujangili wa wanyamapori. Watu hawa wanachukua vipusa na kuvisafirisha nje kinyemela,wanaajiri watu wa kuua wanyama kwa njia haramu. Nchi inapoteza fedha nyingi badala yake wanafaidika wachache tu, wakati  hivi vilipaswa kuwafaidisha wananchi wote.

Pia tunamuona Kashogi akiuza vipuli vya magari na mafuta kwa magendo hata wauza mafuta wengi walificha mafuta n kuyauza kimagendo.

Katika uhujumu uchumi,tumeona jinsi Brown Kwacha alivyoshiriki kuchoma jengo la ofisi yake ili apoteze ushahidi muhimu uliohitajiwa na bunge.

 

9.      UJAMBAZI NA UJANGILI

Mwandishi ameonesha wazi kuwa ujambazi ni tatizo kubwa na unarudisha nyuma maendeleo na kuwafanya watu wapoteze maisha. Mfano mwandishi amemuonesha Omar Mahafudh,mfanyabiashara aliyepamabana kwa muda mrefu licha ya vikwazo kadhaa kukuza biashara yake alivyokufa baada ya duka lake kuvamiwa na majambazi.

Pia mwandishi ameonesha jinsi ujangili ulivyokuwa tatizo sugu na unavyotishia kumaliza wanyama amabao ni kivutio cha watalii na pia ni chanzo cha mapato kwa taifa na jamii. Mfano Brown Kwacha alikuwa ameajiri watu akiwapatia silaha ili wawinde wanyama kiharamu kasha yeye kusafirisha nje vipusa.

 

 

   10. MAPENZI NA NDOA

a)      Kuhusu mapenzi mwandishi ameonesha mapenzi ya aina mbili;

Mapenzi ya kweli (dhati)  na yasiyo ya kweli(yasiyo ya dhati)

-          Katika mapenzi ya kweli mtunzi ameonesha kama ifuatavyo;

Mapenzi ya kweli kati ya Tino na Amani, hawa walikuwa marafiki walioshibana kweli kwani walisaidiana katika shida na raha,tunaona jinsi Amani alivyomsaidia Tino katika kutatua shida ilyompata rafike Tino ya kuumia kwa Cheche,mwishoni Amani aliamua kumsaidia Tino kuiba benki ili Cheche akatibiwe nje.

Mapenzi ya kweli kati ya Tino na Jinja Maloni,pamoja na Tino kuwa masikini aliamua kumchukua Jinja na kuishi naye kwake ili Jinja asiathirike na mji.

Mapenzi ya kweli kati ya Tino kwa familia yake,Tino aliipenda sana familia yake hasa mkewe na watoto wake hasa Cheche,ndiyo maana hata Cheche alipolazwa muda mwingi Tino alikuwa na  msongo wa mawazo na alitumia njia ngumu kuhakikisha anasafiri kwenda kumwona na kumuuguza mwanaye.

-          Mapenzi ya uongo/yasiyo ya kweli

Mapenzi yasiyo ya kweli yameoneshwa kwa;

Kati ya Brown Kwacha na wanawake wake,Kwacha hakuwapenda kidhati wanawake wake bali aliwatumia kama njia ya kujistarehesha tu ndiyo maana aliwabadili kama nguo.

Kati ya Brown Kwacha kwa watoto wake na mkewe,watoto wake walikuwa wakimuogopa baba yao hawakuthubutu hata kumuomba baba yao kitu.

b)     Kuhusu ndoa mtunzi ameonesha ndoa  za uongo na za kweli

-          Ndoa ya kweli

Mtunzi ameonesha ndoa ya Tino na mkewe kuwa ya kweli kwani waliaminiana na kushirikiana katika kulea familia yao hata walipokosea kila mmoja alijirekebisha. Walikuwa pamoja kwa kila hali na hawakusalitiana.

 

 

 

-          Ndoa ya uongo

Ndoa ya Brown Kwacha na mkewe,hawa hawakupendana kwa dhati na hawakuthaminiana wala kukubaliana. Brown Kwacha hakuridhika na mkewe ndiyo maana alikuwa akimsaliti mkewe na hakumshirikisha kwa lolote.

 

 

B; MIGOGORO

Migogoro kdha wa kadha imejitokeza katika riwaya hii kama ifuatavyo;

A)    Mgogoro kati ya Jinja Maloni na vibaka waliokuwa wakimbaka mwanamke vichakani. Jinja aliwataka wamwache lakini walikataa hata hivyo Jinja Maloni alifanikiwa kumwokoa mwanamke Yule baada ya kuwapiga wabakaji wale waliotishia kumpiga mwanzo.

B)    Mgogoro baina ya Tino na kondakta na utingo wa basi. Kondakta na utingo  waliona kama Tino na kwama lake barabarani alikuwa akiwachelesha,na kuamua kushuka kutaka kumpiga Tino ambaye alisimama imara utingo na kondakta wakaogopa na kurudi katika basin a kuondoka.

C)    Mgogoro kati ya vjana waliokuwa wakipigania matenga yalikuwa yakishushwa,vijana hawa walipigana bila kuamuliwa na mtu yeyote mwishowe walichoka na kutazamana kama majogoo yakiyokuwa yakitangaza vita.(uk. 34)

D)    Mgogoro kati ya katibu mkuu wa wizara ya mila na utamaduni na kijana waliopigana katika uzinduzi wa nyumba ya Brown Kwacha,walikuwa wakimpigania mwanamke aitwaye Esther,walipigana mpaka wakatumbukia katika bwawa la kuogelea.

E)     Mgogoro wa kinafsi aliokuwa nao Tino,muda mwingi tangu mwanaye Cheche aumie alikuwa anawaza na kuwazua namna ya kupata fedha za kumpeleka mwanaye nje kutibiwa.

F)     Mgogoro wa kibinafsi aliokuwa nao Brown Kwacha pale alipogundua kuwa bunge linahitaji ripoti kuhusu fedha za kigeni kutoka ofisini kwake alikuwa akiwaza afanye nini juu ya matakwa ya bunge. Pia hakupenda jinsi wanafunzi wa uganga na uuuguzi walivyokuwa wakimtumia kujifunza hasa apale aliolazwa hospitali akiwa na tatizo la kuziba mkojo.

C; UJUMBE/MAADILI

         Mwandishi wa riwaya hii ametoa mafunzo kadhaa kama ifuatavyo;

A)    Rushwa ni adui wa haki,kwamba penye rushwa haki hujitenga mbali. Rushwa ni ufisadi hivyo jamii sharti ipambane kwa kila hali kuhakikisha kuwa rushwa inatokomezwa kabisa. Mfano Brown Kwacha alipokea rushwa ili kutoa huduma aabazo zilikuwa ni haki za watu na wmakubwa kwa maisha ya wananchi walitakiwa kuzipata bila hongo.

B)    Ufisadi wa viongozi ni uhalifu na una madhara kwa wananchi wa kawaida. Jamii inapaswa kutokomeza ufisadi kwa kila hali.

C)    Mapenzi ya dhati na kushirikiana katika jamii ni muhimu sana kw awanandoa,marafiki na familia ili kudumisha amani miongoni mwao na pia kusaidia kufikia malengo ya kimaisha.

D)    Jamii sharti ibadilishe mfumo wa maisha unaomkandamiza mwanamke na asiendelee kuonekana kiumbe duni,tegemezi au chombo cha starehe. Mwanamke athaminiwe na apewe usawa na haki.

E)     Wanajamii sharti waachane na imani za kishirikina badala yake waamini katika juhudi na nguvu zao. Kwani kufanikiwa katika maisha hakuna njia za mkato wala nguvu za giza.

F)     Wanajamii pia wajishughulishe na shughuli na kazi halali ili kujipatia kipato kwani,ujangiili,ujambazi na magendo vinarudisha nyuma maendeleo ya jamii na kuiletea jamii maumivu makubwa.

 

D; MTAZAMO

Mwandishi ana mtazamo wa kiyakinifu

Mwandishi ameainisha kero mbalimbali za wananchi kwa uwazi,ameonesha uozo wa jamii bila kificho wala woga na jinsi viongozi wanavyohusika .

Mwandishi anawanyooshea kidole wananchi kuwa wao ndio hasa chanzo kikubwa cha ugumu wa maisha kwa wananchi hasa kwa ufisadi,urasimu,rushwa na kutowajibika kwao.

E; MSIMAMO

Mwandishi ana msimamo wa kimapinduzi

Mwandishi ameweka bayana matatizo kadha wa kadha yanayomkumba mwananchi wa kawaida,ameonesha chanzo chake na kila anayehusika katika kila tatizo. Mwandishi kwa kufanya hivyo anaamini jamii itazinduka na kuamka na kuapambana na vyanzo vya matatizo hayo.

 

F; FALSAFA

Mwandishi anaelekea kuamini kuwa matatizo makubwa yanayojitkeza katika jamii yanatokana nakusababishwa na kutowajibika,urasimu,rushwa na ufisadi wa viongozi.

 

 

 

FANI

A; MTINDO

-          Riwaya ya Joka la Mdimu imetumia muundo wamasimulizi. Kwani visa vinasimulia kinathari.

-          Pia dayalojia/majibizano imetumika kwa kiasi kidogo kwani tumeona wahusika wakijibizana moja kwa moja katika baadhi ya sehemu. Mwandishi amefanya hivyo ili kuweka uhalisia wa mazungumzo baina ya wahusika.

-          Pia mwandishi kwa sehemu kubwa ametumia nafsi ya tatu,japo kwa sehemu ndogo ametumia nafsi ya pili na ya kwanza.

-          Mwandishi ametumia pia nyimbo katika riwaya hii. Mfano katika riwaya kuna wimbo wa Chaupele..(uk. 70-71)

 B; MUUNDO

-          Riwaya ya Joka la Mdimu ina jumla ya sura kumi(10) ambazo amezipa majina ya wahusika,mahali na matukio yanayobeba kisa kizima cha hadithi katika sura husika.

-          Mwandishi ametumia muundo wa rukia kwani amekuwa akisimulia visa kwa kusimulia matukio mengine na kuyaacha kuelezea matukio mengine katika sura tofauti tofauti.

 C; WAHUSIKA

I)                   AMANI

-          Ni dereva taksi

-          Ni kijana mchapakazi

-          Ana huruma,hekima na busara.

-          Ni rafikiye wa dhati Tino.

-          Alimsaidia Tino katika tukio la kuiba benki.

-          Anafaa kuigwa na jamii

II)                BROWN KWACHA

-          Ni mkurugenzi wa idara ya fedha za kigeni

-          Ni malaya

-          Anahudumia watu ofisini kwa upendeleo hasa wanawake

-          Ni mpenda rushwa.

-          Anajihusisha na magendo na ujangili

-          Hafai kuigwa na jamii

III)             TINO

-          Ni mvuta kwama

-          Ni baba wa watoto watatu,Cheche,Tabu na Subira.

-          Ni jasiri sana

-          Ni mchapa kazi na mwanamichezo.

-          Anafaa kuigwa

 

IV)             JINJA MALONI

-          Ni mtu mkakamavu na asiye mwoga.

-          Hufanya kazi kama za kupakua vyoo na kuchimba makaburi

-          Ana upendo na moyo wa kujitoa hasa inapokuja suala la kuokoa mtu

-          Anapenda muziki.

V)                DAKTA MIKWALA

-          Ni daktari bingwa wa mifupa

-          Ni mlevi

-          Ni mpenda rushwa/hongo

VI)             SHIRAZ BHANJ

-          Ni mfanyabiashara mkubwa.

-          Ni mwajiri wa Amani

-          Ni rafikiye Brown Kwacha

-          Ni mtoa rushwa

VII)          CHECHE

-          Ni mtoto wa kiume wa Tino

-          Alivunjika kiuno katikamichezo ya  sherehe za uhuru

-          Ana tabia njema

-          Ni mcheshi,mdadisi na mwanamichezo

-          Alipendwa sana na watu.

 

Wahusika wengine ni kama Zitto, Leila,Josephine,Pamela,Mwema na wengineo.

D; MATUMIZI YA LUGHA

Lugha ilyotumika ni ya kawaida iliyosheheni tamathali za semi na mdinu nyingine za kisanaa.

i)                    MISEMO

-          Asiye na bahati habahatishi (uk. 10)

-          Tandu kwenda mbele na nyuma ndiyo hulka yake(uk. 25)

-          Asiyezika hazikwi(uk.48)

-          Mmetupa jongoo na mtiwe(uk.64)

ii)                  METHALI

-          Asilolijua mtu ni usiku wa giza (uk.77)

-          Ukiona mwenzio ananyolewa tia maji(uk. 83)

-          Mtaka waridi sharti avumilie miiba(uk. 98)

-          Biashara haigombi(uk. 99).

iii)                MATUMIZI YA LUGHA NYINGINE

a)      Kiingereza

-          Mission to Seamen please(uk. 24)

-          Hey man you will pay extra dollars(uk. 24)

 

b)     Kiarabu

-          Inna lillahi wa inna ilahi rajiunna! (uk. 41)

iv)                TAMATHALI ZA SEMI

a)      Tashbiha

-          Zepher 6 ile iliunguruma kama samba aliyeghadhibishwa (uk. 9)

-          Wote walikimbilia kule wakiminyana kufa au kupona kama kaa wanavyogombea mavi ya mvuvi(uk. 21)

-          Maduka makubwa yalichipua  mithili ya uyoga (uk. 26)

-          Miguu yake ilikazana mithili ya upinde uliotaka kufyatuliwa(uk. 33)

b)     Tashihisi

-          Utumbo ulimlaumu(uk. 12)

-          Mvua ikarindima kwa kiburi na kuviadhibu vibati vibovu(uk. 27)

-          Lakini hata fikra nazo zilikuwa kama zimempiga chenga(uk.4)

c)      Sitiari

-          Sote kobe (uk. 72)

-          Sarahange wetu mbogo kweli siku hizi(uk. 15)

v)                  MBINU NYINGINE ZA KISANAA

a)      Onomatopea/tanakali sauti

-          Saa mezani iliendelea kugonga ” ta ta ta” (uk 04)

-          Akazungusha ufunguo wa gari lake na kutaka kuliwasha lakini ikatokea sauti kali fupi “ta nye nye”(uk. 10)

b)     Takriri

-          Funga,shinda! Funga,shinda! Sauti za mashabiki zikarindima tena(uk. 56)

-          Shinda! Shinda! Shinda! Kibanda kilitetemeka tena (uk.55)

-          Shetani! Oyee! Shetani! Oyee! Shetani chinja! (uk. 58)

 E; MANDHARI

Riwaya hii imejengwa katika mandhari ya mjini. Mwandishi ametumia majina ya miji kama Mindule,Sega,Boko na Kwale ambayo ameitaja kwamba ni mjini.

Mandhari haya yanaweza kugusa nchi zote zinazoendelea ambapo kuna hali ngumu ya uchumi na matatizo ya ufisadi na urasimu sambamba na uzembe wa viongozi.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

F; JINA LA KITABU

Jina la kitabu JOKA LA MDIMU ni jina ambalo limejengwa kwa lugha ya picha. Joka la Mdimu ni aina ya nyoka hatari apendye kuishi katika miti ya kijani kama  midimu. Nyoka huyu huwa na rangi ya kijani hivyo si rahisi sana kumwona kwa macho harakaharaka kwani hufanana kwa kiasi kikubwa na miajani ya miti aliyomo. Nyoka huyu ni hatari sana kwa maisha ya watu.

Joka la Mdimu  limrtumika kuwakilisha viongozi hatari waliopo katika jamii kama fisadi Brown Kwacha.

Jina la kitabu linasadifu yaliyomo kwani kitabu kinazungumzia mafisadi na walanguzi,wahujumu uchumi,watoa rushwa na wapokeaji na wafanya magendo. Hawa hasa ndiyo majoka yenyewe kwani tunaishi nao atika jamii wakijifanya ni wanajamii wa kawaida lakini undani wa maisha na shughuli zao ni hatari sana.

 

KUFAULU NA KUTOFAULU

KUFAULU

Kimaudhui mwandishi amefaulu kuelezea matatizo yanayoikabili jamii. Ameeleza kwa uwazi bila kuficha namna maisha ya watu wa tabaka la chini yalivyo magumu wakati viongozi na wafanyabiashara wakifurahia maisha. Ameeleza kwa dhati matatizo ya uhujumu uchumi,urasimu na ufisadi yanavyokuwa tatizo kw amaendeleo.

Kifani mwandishi amefaulu kutumia lugha amabayo amewapa wahusika kulingana na uhusika wao. Ametumia tamathali za semi ambazo zinabeba dhamira halisi ya mwandishi.

KUTOFAULU

Kimaudhui mwadishi ameshindwa kutoa masuluhisho ya matatizo anuwai na hata aliptoa basi masuluhisho yamekuwa ni ya kihalifu zaidi. Kwa mfano Brown Kwacha alipogundua hesabu za ofisi yake zinahitajika bungeni basi aliamua kchoma moto ofisi yake,pia Tino alipoona kuwa ni vigumu kupata pesa za kumpeleka mwanaye nje aliamua kwenda kuiba fedha benki.

 

 

 

Mwisho

 

 

4 comments:

  1. Good job nimeipenda Sanaaaaaaa๐Ÿ˜€๐Ÿ˜€๐Ÿ˜€๐Ÿ˜€

    ReplyDelete
  2. unabainishaje wahusika katika joka la mdimu

    ReplyDelete
  3. Tunaomba muzidi kutusaidia wanafunzi kusoma online na mutufahamishe mbinu za kujibu maswali ya mtihani
    Asante saba

    ReplyDelete
  4. Live Casino Site, Offers & Bonuses | LuckyClub.live
    Welcome to Lucky Club! Live Casino Site, Offers, & Bonuses. Live Casino Site. Play for real and get exclusive free luckyclub.live chips & VIP rewards!

    ReplyDelete