Total Pageviews

Friday, 27 January 2017

Imeandaliwa na Kimario L. na Chabai M.

HISTORIA YA SHAABAN ROBERT KWA UFUPI

Shaaban Robert alikuwa mwandishi mashuhuri wa kazi za fasihi ambazo ni ushairi na nathari. Alizaliwa tarehe 01.01.1909 huko Vibambani kusini mwa Machui mkoani Tanga, Tanzania. Alifariki tarehe 22.06.1962 na akazikwa Machui. Ni miongoni mwa Watanzania waliochangia kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili kupitia kazi zao za kifasihi. Alipata elimu ya dini ya Kiislamu huko mkoani Tanga mpaka alipohamia Dar es salaam wakati huo ikijulikana kama Mzizima, alijiunga na kisomo cha darasani kuanzia mwaka 1922-1926 na akafaulu vizuri katika masomo yake na kupewa shahada ya kuhitimu.

Kutokana na juhudi zake aliweza kuwa mwanachama wa Kamati ya Lugha ya Afrika Mashariki, Bodi ya Lugha Tanganyika, Chama cha Wanafasihi wa Afrika Mashariki pia mwanachama wa mamlaka ya jiji la Tanga. Katika maisha yake pia aliwahi kufanya kazi idara ya forodha Pangani, Idara ya Wanyama, Afisi ya mkuu wa jimbo Tanga na Afisi ya kupima nchi.

Kazi iliyompa jina ni kazi ya uandishi wa nathari na ushairi.

Katika uchambuzi wetu tunahakiki utenzi wake wa Mapenzi Bora.


UTANGULIZI

Mapenzi bora ni utenzi ulioandikwa na Shaaban Robert mwaka 1958.Utenzi huu una beti 700 ,ambazo lengo lake ni kuiadilia jamii juu ya maana,sifa,faida na hasara za kukosa mapenzi bora. Mwandishi wa kitabu hiki anasema,kusudi ni kuandalia mahitaji ya watu waliofikia fahamu ya kuwaza na kuhoji neno au kitu au tendo kwa akili ingawa haitakuwa vibaya kikisomwa na watu wowote ambao hawajafikia upeo kama huo wa kupenda, kujiweka tayari kwa zamu yao.Pia ni kwa watu ambao wana dhana kwamba,mapenzi si kitu cha maana, wanaonywa kuwa wanapata hasara kubwa kwa kupitwa bila kujua uzuri na fahari, heshima na utukufu ambao hustahili wao wenyewe. Ni kwamba wanamiliki majohari wasiyojua thamani yake. Pia anawaandikia watu wanaodai kuwa,mapenzi karaha  kuzungumzwa. Anadai wanachekesha si kidogo. Mwisho  anasisitiza kuwa mapenzi ni jambo moja katika mambo yaliyo muhimu katika wajibu wa mwanadamu.

DHAMIRA

Samwel na wenzake (2013:126) anasema dhamira ni mada, lengo, kusudi, wazo kuu linalozungumzwa na shairi/ kazi ya sanaa. Mashairi huweza kuwa na dhamira za kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata kiutamaduni. Katika kazi ya fasihi kunaweza kuwa na dhamira kuu na dhamira ndogo ndogo.

DHAMIRA KUU

1.      MAPENZI YALIYO BORA

Katika kuifafanua dhana ya mapenzi bora mwandishi S. Robert amefafanua,maana ya mapenzi bora, faida za kuwa na mapenzi bora pamoja na hasara za kukosa mapenzi bora.

A.    Kwanza kabisa mtunzi ametuonesha maana ya mapenzi bora ni ipi;

·         Kwa mujibu wa mtunzi,mapenzi bora ni mapenzi ya kumcha Mungu,kwani ndiye Muumba wa ulimwengu na ndiye anayeamua jaala za wanadamu. Hivyo ni vyema kumpenda Mwenyezi Mungu.

             Mfano katika ubeti wa 122 anaposema;

         Tusihini walimwengu,

              Mapenzi tumpe Mungu,

        Naye atatupa fungu,

          Katika wake wenezi.”

·         Pia mtunzi anasema kuwa mapenzi yaliyo bora ni yale ya kupendana wenyewe kwa wenyewe bila kubaguana au kwa kuangalia tofauti zetu za mambo kama vile rangi, jinsia, kabila na hali za kiuchumi.

            Mfano katika ubeti wa 123 anaposema;

           Tupendane na wenyewe

Tofauti tuondoe,

Amani itushukie,

          Mapenzi tufanye ngazi.”


             Pia hili limedhirika katika beti za 116,117 na 118.

B.     Katika kuelezea swala la mapenzi bora mwandishi amebainisha sifa mbalimbali za mapenzi bora kama ifuatavyo;

·                     Anasema mapenzi ni kama pambo la moyo,kwamba mapenzi bora ni jambo linaloupendeza moyo na kamwe haliishi uzuri wake.

Mfano katika ubeti wa 467

      “Mapenzi pambo la moyo,

Ni furaha kuwa nayo,

   Mapenzi hushinda cheo,

                                                Hata pato la ghawazi.

·                     Mapenzi ni kitu cha thamani kubwa na endapo tukiyapoteza tutaingiwa na gharama kubwa sana kuyarudisha,

Mfano katika ubeti wa 103-104 kama anavyosema;

103. “Wote wapige mayowe,

Mapenzi wayalilie,

  Kwa kutaka yarejee,

 Na kurudi hayawezi.”

                                          104. “Watayataka kwa pesa,

Yawape tena fursa,

Kitu walichokifyosa,

Huwaje tena kipenzi!”

·                     Mapenzi bora hayaambatani na aina yoyote ya chuki,na pia yenyewe ni kama dawa iondoayo chuki. Mfano katika ubeti wa 471

“Kitu hiki ni mithaki,

Kwa waelewa haki,

      Mapenzi dawa ya chuki,

    Kwa watu wavumilizi.”

·                     Mapenzi bora ni kitu kisicho na kipimo,huwezi kuyapima wala kuyalinganisha na kitu chochote hata dhahabu. Mfano ubeti wa 473;

“Hushinda hata dhahabu,

 Yapimwapo kwa hesabu,

                                              Mapenzi yana ajabu,

                                             Hayapimiki kwa wazi.”


C.    Lakini pia katika utenzi huu ameonesha faida jamii izipatazo endapo itashikilia na kuwa na mapenzi bora;


·                     Watu wakiwa katika mapenzi bora wote hujiona wa aina moja na hawazioni tofauti zao za mambo kama vile rangi wala hawajihisi kubaguliwa.

Mfano katika ubeti wa 147

“Mapenzi wanayo mengi,

Wanadamu kila rangi,

                                                Lakini hayawaungi,

Kwa sera ya ubaguzi.”

·                     Kukiwa na mapenzi bora haki itatawala katika jamii na hapatakuwa na dhuluma na watu wataheshimiana.

Mfano katika ubeti wa 627-631

                                           628.  “Wanadamu kwa wanyama,

             Na wadudu wa kuuma,

    Walisafiri salama,

               Kwa imani na mapenzi.”

·                     Mapenzi ya kweli humfanya mtu ajione kuwa hana haja ya mali wala utajiri. Anasisitiza kuwa penye dhiki na msiba marafiki huwa haba na pia mfiwa huweza hata kukosa wa kumshauri,kinachoweza kuondoa shida hii basi ni mapenzi bora tu. Mfano katika ubeti wa 271-274

Katika ubeti wa 271 anasema

“Kama mapenzi ya kweli,

                                                           Hayana haja ya mali,

Na wala hayendi mbali

Siku ya kuja majonzi.”

·                     Mapenzi bora huondoa matatizo mbalimbali yaliyopo katika jamii,kama vile chuki,choyo,uchokozi,ghasia,wivu na utovu mwingine wa nidhamu. Kwamba katika ulimwengu huu uliojaa ghasia mapenzi bora ndiyo kimbilio.


Mfano katika ubeti wa 66

“Ulimwengu kama huu,

    Wenye mashaka makuu,

                                                 Kimbilio na nafuu,

  Ni palipo na mapenzi.”

·                     Mapenzi bora huleta amani na utulivu. Mapenzi bora huleta mwafaka na kuondoa mshaka na hivyo furaha kutawala katika jamii.

Mfano katika ubeti wa 552-557

552. “Ni kitu chenye Baraka,

                  Na mambo huwa mwafaka,

        Halizuki la mashaka,

       Wala neno la tatizi.”

D.    Aidha mwandishi ameonesha hasara jamii inazoweza kuzipata kwa kukosa mapenzi bora kama ifuatavyo;

·                     Mapenzi yakimezwa na chuki huleta kutokuelewana na kupotea kwa amani katika jamii,tena anasisitiza kuwa chuki ni kitu hatari kama moto katika jamii.

Mfano katika ubeti wa 333-35

                                            333. “Chuki inashinda moto,

   Ikisadifu mateto,

        Chuki ni kitu kizito,

        Kueka hatukiwezi.”

·                     Kukosekana kwa mapenzi bora ni chanzo cha masikitiko,masumbuko,maudhi na ghasia/fujo katika jamii. Mfano katika ubeti wa 195-198

195.  “Kitu chenye maudhiko,

          Na fujo na masumbuko,

   Dhiki na masikitiko,

        Kuwapo ni pingamizi.”


·                     Kukosekana kwa mapenzi bor akatika jamii huleta ubaguzi,hufanya watu wadhulumiane.


 Mfano katika ubeti wa 126.

“Ubaguzi ni husuda,

Wala hauna faida,

     Unadhuru kila muda,

Katika kila kizazi.”   


2.      DHAMIRA NDOGONDOGO

A.    CHUKI

Mtunzi ametuonesha kwamba chuki sio jambo la kukumbatiwa na ina madhara makubwa kama ikiendekezwa na pia ameifananisha na laana, huleta maudhi na huweza kuharibu mambo kwa muda mfupi.

Mfano katika ubeti wa 335,336 na 345

336. “Chuki madhara ya dhati,

 Afadhali ya mauti,

       Ni faradhi kwa umati,

           Chuki inanyong’onyezi.”



B.     CHOYO

Mwandishi ametuonesha kwamba choyo ni tatizo kubwa,humfanya mtu asione na asiwe na mapenzi kwa wenzake na pia huleta uadui, choyo humfanya mtu akawa mpumbavu. Mfano katika ubeti wa 364-378

364. “Akiwa katika choyo,

          Mtu fahamu hinayo,

     Kadiri hali iwayo,

           La mapenzi haliwezi.”


C.    MATABAKA

Mtunzi ameweka wazi namna jamii yetu ilivyo na matabaka na hasa tabaka la wenye nacho yaani matajiri na wasio nacho yaani masikini. Haya yamebainishwa katika ubeti wa 95 na 289.

Mfano katika ubeti wa 95

                                                          “Maskini na tajiri,

           Watu wa kila umri,

         Kulia watakithiri,

            Kama hili hubarizi.”

D.    KULEWA SIFA

Mtunzi amezungumzia suala la mtu kulewa sifa na jinsi jambo hili lilivyo na madhara makubwa. Anasema mtu akilewa sifa humfanya ahadaike,alaghaike na huweza kumletea matatizo mengi. Mfano katika ubeti wa 211,212 na 215.

                                            212.  “Mimi sifa za dunia,

Sina haja kusikia,

  Sababu zinahadaa,

             Na wingi wa mapinduzi”.


E.     ULEVI

Mtunzi amezungumzia suala la ulevi wa pombe na mihadarati,ameonesha kwamba ulevi wa vitu hivi humfanya mtu asiwe na mawazo mema,fikira zake zigure,awe bwege,akili zisimtoshe na kupungua kwa fikra.

 Mfano katika ubeti wa 49-58

Ubeti wa 52.

52. “Nahisi kalewa mbege,

          Ni sawa na mtu bwege,

             Mapenzi tunda za ndege,

           Wanayama na sisimizi.”

UJUMBE

Samwel na wenzake (2013:126) wanasema ni yale mambo ambayo mshairi angependa hadhira ijifunze ili kuweza kufanikisha misimamo iliyojengwa na msanii huyo.

 Mwandishi S. Robert ameibua ujumbe wa aina tofauti katika utenzi wake huu kama ifuatavyo;

                                i.            Kila mwanajamii bila kujali ni masikini au tajiri anahitaji mapenzi ya dhati yaliyo bora,kwani mapenzi ni muhimu kwa matabaka yote.  Mfano katika ubeti wa 95

                              ii.            Mapenzi ya kweli ni tiba,uguzo kwa wagonjwa na ni faraja kwa yatima.  Kwa kuwa mapenzi ni muhimu kwa kila mzunguko wa maisha. Mfano ubeti wa 251-252

                            iii.            Mapenzi ya dhati yaliyo bora kwa mwanadamu yeyote ni muhimu kwani pakikosekana mapenzi kwa muda mfupi,kwa mfano hata kwa muda wa saa moja tu wanadamu watakufa kwa majonzi. Mfano ubeti wa 323

                            iv.            Mapenzi ya kweli huondoa uhasama,tuhuma na fitina. Palipo na mapenzi ya kweli panakuwa hakuna migongano. Mfano kama inavyooneshwa katika ubeti wa 137.

                              v.            Chuki haifai hivyo sharti itokomezwe kabisa,na hakika ina madhara makubwa.  Chuki huleta hila na ukabila na huleta aibu.Mfano katika ubeti wa 127 na 132.


FALSAFA

Wamitila (2003:45) anasema falsafa ya mwandishi ni mawazo au wazo alilo nalo juu ya kile anachokiamini kuwa kina msingi unaotawala maisha. Tunapotaja falsafa tunarejea juu ya mawazo aliyo nayo juu ya maisha ambayo yanajitokeza katika mandishi yake.

Mwandishi Shaaban Robert  anaamini kuwa mapenzi bora,yaani mapenzi ya kupendana wanajamii wote bila kujali tofauti zetu za rangi,dini,kabila na tofauti nyingine pamoja na kumpenda Mwenyezi Mungu yataifanya dunia iwe mahala pazuri sana pa kuishi na pia Mwenyezi Mungu atatupatia thawabu.


MSIMAMO

Kwa mujibu wa Samwel na wenzake (2013:126) wanasema msimamo pia ni mtazamo wa mshairi. Msimamo ni jinsi mshairi anavyochukulia mambo katika ulimwengu au jamii husika anayoisawiri.

Katika utenzi wa Mapenzi bora mwandishi ametumia mitazamo yote miwili yaani wa kidhanifu na kiyakinifu. 

Kiyakinifu mwandishi ameonesha kwamba mapenzi ya kweli ni muhimu kwa maendeleo ya nyanja zote za maisha ya binadamu. Hii ni kutokana na jinsi alivyolizungumzia suala la mapenzi ya kweli na nafasi yake katika kuleta maendeleo,amani,kuondoa matabaka,ubaguzi na kupambana na tuhuma na fitina kwa wanajamii.

Kidhanifu, Gibbe(1978:5) anaposema washairi wa kale walisisitiza sana umuhimu wa kupendana. Mapendo waliyosisitiza yalikuwa mbinu mojawapo ya kuwapofusha wanyonge ili wasipambane kitabaka bali wapendane na matajiri.  Maskini, yaani wanyonge, wasiwaonee wivu matajiri kwani Mungu ndiye kawapa,kwa hiyo kila mmoja aridhike na alichopewa.

Katika utenzi wa Mapenzi Bora, Shaaban Robert anasisitiza watu wapendane, waridhike na hali zao, kwani asiyeridhika na hali yake hupata tamaa “mbaya”. Kwahiyo mapenzi bora aliyokuwa anayasisitiza S. Robert yalikuwa mapenzi “duni”, kwani katu hayangewasaidia wanyonge kujikomboa.

FANI

            MUUNDO

Senkoro (2011:23) anasema muundo wa kazi ya fasihi ni mpango na mtiririko wa kazi hiyo kwa upande wa visa na matukio. Hapa tunachunguza jinsi msanii au mtunzi wa kazi ya fasihi alivyofuma, alivyosuka, alivyounda na alivyounganisha tukio moja na lingine, kitendo kimoja na kingine, wazo na wazo, sura moja na nyingine, ubeti na ubeti hata mstari wa ubeti na mwingine.

Mtunzi  S. Robert  ametumia muundo ambao beti zake zimeundwa kwa mishororo minneminne yaani tarbia,ambapo kila mshororo una mizani nane,vina vya mwisho vilivyojitokeza katika utenzi huu ni ‘zi’ na ‘nzi’.

MTINDO

Njogu na Chimerah(1999:93) wanasema kuwa hakuna njia moja ya kuuelezea mtindo. Lakini kwa ujumla twaweza kusema kwamba “mtindo ni tabia ya utungaji inayopambanua mtunzi mmoja na mwingine.”

Katika diwani hii mtunzi ametumia mtindo wa usahiri wa monolojia,  kwani utenzi huwa ni simulio juu ya jambo fulani lakini kwa lengo la kuiadilisha jamii, aidha mtunzi ameandika beti 700 akifafanua kiundani suala la mapenzi bora.

Kila ubeti una mishororo minne yenye mizani nane na vina vinavyofanana katika mistari mitatu ya mwanzo ya kila ubeti.

MATUMIZI YA LUGHA

Tamathali za semi

Senkoro (2011:12) anasema ni maneno,nahau au sentensi ambazo hutumiwa na wasanii wa fasihi ili kutia nguvu katika maana, mtindo na hata sauti katika maandishi ama kusema. Hizi wakati mwingine hutumiwa kuwa njia ya kuipamba kazi ya fasihi na kuongeza utamu wa lugha. Zifuatazo ni tamathali za semi katika utenzi wa Mapenzi Bora;

                                a)      Sitiari

Senkoro (2011:15) anasema hii ni sawa na tashbiha hulinganisha vitu ama watu bila kutumia viunganishi-linganishi vya mithili ya, mfano wa, sawa na, kama na vinginevyo.

ü  Mapenzi ua la moyo  mfano ubeti wa 161

Hapa mtunzi alikuwa na maana kwamba mapenzi huufurahisha na kuupendeza moyo wa aliye nayo.

ü  Kupendana ni ungwana mfano katika ubeti wa 206

Hapa mtunzi alikuwa na maana kuwa kupendana ni jambo la busara kwa kila mmoja.

ü  Chuki mwanawe ni kondo mfano katika ubeti 280

Hapa mtunzi alikuwa na maana kwamba chuki haina maana na inarudisha nyuma juhudi za kusonga mbele.

ü  Maisha ni utelezi mfano katika ubeti wa 641

Hapa pia mwandishi alikuwa na maana kwamba maisha ni kama jambo linaloweza kukatika muda wowote.

b)     Tashihisi

Senkoro(2011:17) anasema kwamba wakati mwingine tamathali hii huitwa fasili ya binadamu. Kwa tamathali hii vitu visivyo na sifa walizo nazo watu huepwa sifa hizo.

ü  Tunachekwa na wadudu,wajinga wa kuabudu mfano katika ubeti wa 201

Mtunzi amewapa wadudu uwezo wa kucheka kama binadamu, kwamba tusipoyazingatia mapenzi yaliyo bora hata wadudu watatucheka.

ü  Chuki ilie kwa wivu mfano katika ubeti wa 583

Mwandishi ameipa chuki uwezo wa kulia na kuwa na wivu kama binadamu.

ü  Kondoo na mbwamwitu,hawakuteta kwa kitu mfano katika ubeti wa 630

Aidha, mwandishi amewapa uwezo kondoo na mbwa mwitu uwezo wa kuteta. Kuteta ni jambo aliwezalo binadamu peke yake.


c)      Tashibiha

Senkoro (2011:17) anasema katika tamathali hii watu ama vitu viwili au zaidi hulinganishwa na watu ama vitu vingine kwa kutumia maneno kama, mithili, kama kwamba, mfano wa, na mengine ya aina hiyo.

Katika utenzi wa Mapenzi Bora tashbiha zifuatazo zimejitokeza;

ü  Mapenzi kwa mwanadamu,kama mshipa na damu, mfano katika ubeti wa 86

Mtunzi amelinganisha mapenzi kwa wanadamu kama damu na mishipa vinavyotegemeana,kwamba kimoja hakiwezi kuwepo na kikafanya kazi bila mwenzake.

ü  Yawambe kama mimea katika ubeti wa 242

Hapa mtunzi anahamasisha kwamba mapenzi sharti yakuwe na kuimarika kama mimea

ü  Chozi litatiririka,mfano kama gharika katika ubeti wa 278

Mtunzi analinganisha utiririkaji wa machozi ya kukosa mapenzi na gharika. Anaonesha jinsi machozi yatakavyokuwa mengi.

ü  Twanuka kama kutuzi katika ubeti wa 298

Mwandishi anaonesha namna wanajamii wasio na mapenzi wanavyoweza kuonekana kwamba wananuka kama kutuzi.

d)     Mubaalagha

Senkoro (2011:12) anasema kuwa hii hutia chumvi kuhusu uwezo wa viumbe, tabia zao na kuhusu sifa zao kwa madhumuni ya kuchekesha au kusisitiza.

Katika utenzi mifano kadhaa imeonekana kama vile;

ü  Nyuso zote zitatota,kwa bahari ya machozi katika ubeti wa 93

Mwandishi ametia chumvi katika hili kwani hata mtu alie kwa kiasi gani hawezi kupata bahari ya machozi.

ü  Nyuso zikifanya mito, ya bahari ya machozi katika ubeti wa 94

Aidha hapa mwandishi pia ametia chumvi, kwani uso hauwezi kufanya mto na kuwa na bahari ya machozi.

          MBINU NYINGINE ZA KISANII

a)      Takriri

Senkoro (2011:16) anasema ni marudiorudio kwenye sentensi au kwenye usemi ambayo nia yake ni kusisitiza ijapokuwa kwa kawaiida hayahitajiki sana na huweza kukirihisha.

ü  Tuna “tata na tatizi”katika ubeti wa  296 na 297

ü  “Choyo” katika beti za 364 hadi 385

ü  “Chuki” katika beti za 330 hadi 336

b)     Inkisari

Ni mbinu ambayo kwayo maneno hufupishwa kwa malengo ya kuleta urari au idadi ya mizani zitakiwazo. Mfano katika utenzi wa Mapenzi Bora

ü  Neno “dumu” katika mstari huo lilitakiwa kuwa neno “kudumu” katika ubeti wa 92

ü  Neno “upuzi” hapa neno hili lilipaswa kusomeka “upuuzi” katika ubeti wa 240

c)      Mazida

Ni mbinu ya kisanaa ambayo kwayo mtunzi hurefusha neno kwa madhumuni ya kupata vina au idadi ya mizani azitakazo. Mfano katika utenzi huu ni;

ü  Neno ”zamani” katika mstari usemao “watu wa zamani hizi ikiwa na maana ya “zama hizi” katika ubeti wa 98

ü  “Wataalamizi” katika ubeti wa 648 likiwa na maana ya “wataalamu”

Mbinu hizi za kifani zimepelekea kuibuliwa kwa maudhui mbalimbali pamoja na kuifanya kazi hii iwe na mvuto wa kipekee.

 JINA LA KITABU

Jina la kitabu linasadifu/linaendana kabisa na yaliyomo katika kitabu kitabu hiki kwani toka mwanzo hadi mwisho wa kitabu mwandishi anajadili na kuonesha maana ya mapenzi bora, sifa za mapenzi bora, faida na hasara za kukosekana kwa mapenzi bora katika jamii yoyote.

KUFAULU KWA MWANDISHI

KIFANI

Mwandishi aefaulu sana kutumia lugha rahisi na Kiswahili sanifu,na maneno aliyoona yatawawia magumu wasomaji wake ameamua kuyaorodhesha nyuma yaani mwishoni mwa utenzi wake na kuyatolea maana.

Pia mwandishi amefaulu kwani ametumia tamathali za semi kwa wingi kama vile tashibiha, tashihisi, sitiari na mubalagha pamoja na mbinu nyingine za kisanaa.

Pia ameweza kuoanisha vipengele vya fani kiasi kwamba vikawiana na maudhui yaliyomo kwenye utenzi wake.

KIMAUDHUI

Mwandishi amefaulu pia katika upande wa maudhui hasa ukizingatia kwamba utenzi huu unaitwa “MAPENZI BORA” ameweza kuonesha umuhimu hasa wa kudumisha mapenzi bora, lakini pia akaweka wazi kwamba mapenzi yenyewe yaliyo bora ni yapi hasa, na pia akaeleza wazi yale yanayoweza kuwakumba wanadamu wasipozingatia na kuwa na mapenzi ya kweli yaliyo bora.

KUTOFAULU

KIMAUDHUI

Katika kipengele hiki kwa kiasi kidogo hajafaulu kwa sababu anasisitiza watu wapendane, waridhike na hali zao, kwani asiyeridhika na hali yake hupata tamaa “mbaya”. Kwahiyo mapenzi bora aliyokuwa anayasisitiza S. Robert yalikuwa mapenzi “duni”, kwani katu hayangewasaidia wanyonge kujikomboa. (Gibbe 1978:6)

MAREJELEO

Gibbe, A.G, (1978), Shaaban Robert: Mshairi, Dar es Salaam, Taasisi ya Chunguzi

wa Kiswahili.

Njogu, K. na R. Chimera (1999) Ufundishaji wa Fasihi: Nadharia na Mbinu. Nairobi, Kiswahili Tertiary Publishing Project.

Robert, S, (1958), Mapenzi Bora, Dar es Salaam, Mkuki na Nyota Publishers Limited.

Samwel, M na wenzake, (2013), Ushairi wa Kiswahili, Mwongozo kwa Walimu wa Kiswahili na diwani ya MEA, Dar es Salaam, Mevelli Publishers and Method Samwel.

Senkoro F. E. M. K. (2011), Fasihi, Dar es Salaam, KAUTTU Limited

Wamitila K. W. (2003) Kichocheo cha Fasihi: Simulizi na Andishi. . Nairobi: Focus Publications Ltd.

No comments:

Post a Comment