Total Pageviews

Saturday 28 January 2017

NADHARIA YA MWITIKO WA MSOMAJI/UPOKEZI KATIKA TAMTHILIYA YA NGUZO MAMA

UTANGULIZI
Katika insha hii tutahakiki tamthiliya ya NGUZO MAMA iliyoandikwa na Penina Mhando mwaka 1982 kwa kutumia nadharia ya mwitiko wa msomaji. Katika kulijibu swali hili tutaanza kwa kufafanua istilahi muhimu zijitokezazo katika swali yaani wahusika wa kazi ya fasihi,dhana za wakati,muktadha na elimu. Kisha tutaifafanua nadharia ya mwitiko wa msomaji na kuwajadili wahusika wanaojitokeza katika tamthiliya ya NGUZO MAMA kwa kutumia nadharia tajwa kwa kuzingatia vipengele vya wakati,muktadha na elimu ya msomaji.
Senkoro (1982:08) anasema, wahusika wa kazi ya fasihi ni watu ama viumbe waliokusudiwa wawakilishe tabia za watu katika kazi ya fasihi.
Pia Msokile(1992:   ) anasema wahusika ni watu au viumbe katika kazi ya fasihi waliokusudiwa kuwakilisha tabia za watu katika maisha halisi. Wahusika katika hadithi za mapokeo na hadithi fupi kwa kawaida huwa ni wanyama, wadudu,mashetani na mizungu.
Wamitila(2003:123) anaeleza kuwa mhusika ni kiumbe anayepatikana katika kazi ya kifasihi na ambaye anafanana na binadamu kwa kiasi fulani. Wasifu wa mhusika unategemea mkabala uliopo.kazi zinaegemezwa katika mitazamo ya kihalisia na zinamsawiri mhusika kwa namna inayokaribiana sana na binadamu katika ulimwengu wa kawaida.
Hivyo tunaweza kusema kwamba,wahusika ni viumbe hai na visivyo hai ambavyo hutumiwa katika kazi za kifasihi ili kuwakilisha tabia halisi za binadamu.
TUKI(2013:630) wanaeleza kwamba wakati ni muda.majira,mwia,wakaa au wasaa. Katika kazi hiidhana ya wakati itachukuliwa kama kipindi fulani cha utokeaji wa tukio.
Msokile(1992:    ) anafasili muktadha kuwa ni mazingira au hali inayoathiri maana ya neno,sentensi au kazi ya sanaa.anaongeza kuwa kazi yoyote lazima iathiriwe na muktadha. Aidha dhana muktadha katika kazi hii litatumika kama mazingira au hali ya utokeaji wa jambo kama vile kisiasa, kijamii na kiuchumi.
TUKI(2013:17) wanasema elimu ni mfumo wa mafunzo yanayopatikana shuleni,vyuoni au maishani, ni taaluma. Katika kazi hii istilahi elimu itatumiwa kumaanisha uwezo au upeo wa  fikra za mtu kutokana na taaluma yake.


Nadharia ya mwitiko wa msomaji
Huu ni mkabala wa kifasihi ambao matilaba yake ni kuwaelezea wasomaji au wasikilizaji wa kazi ya fasihi namna wanavyoweza kuisoma na kuielewa kazi ya fasihi kutokana na elimu yao,mazingira na wakati.
Wafula na Njogu (2007:85) wanasema ni nadharia inayosughulikia upokeaji wa matini za fasihi kuhusu ulimbwende na mitizamo ya kisaikolojia. Kimapokeo msomaji huwa na mawazo juu ya matini anayopitia. Kutokana na tajiriba ya usomaji,msomaji hupata hisi maalumu. Utunzi na upokeaji wa sanaa hushirikishwa sana na hisi kwa mujibu wa imani na nadharia za kilimbwende. Hizi ndizo humpa mwanasanaa msukumo wa kutunga. Vilevile,msomaji anatazamiwa kupokea kazi ya fasihi kwa kuzingatia mielekeo yake binafsi.
Lobo(2015:13) anasema nadharia ya mwitiko wa msomaji inafafanua mahusiano yaliyopo baina ya wasomaji na matini ili kuonesha maana ya kazi ya fasihi.(tafsiri yetu).
Kwa mtazamo wetu,huu ni mkabala wa kifasihi ambao matilaba yake ni kumwelezea msomaji au msikilizaji wa kazi ya fasihi na namna wanavyoweza kuisoma na kuielewa kazi ya fasihi na kuipa maana kutokana na elimu,historia,mazingira yao na hata msimamo na mtazamo wao katika maisha.
Wafula na Njogu(2007:85) wanasema waasisi na watetezi wakuu wa nadharia ya mwitiko wa msomaji ni Stanley Fish(1980), Jane Tompkins(1980) na Wolfgang Iser(1974,1978).
Anderson (2012:06-07) aliwagawa wananadharia wanaosimamia nadharia hii katika makundi matatu. Kundi la kwanza ni wale wanaoona kwamba mwitiko wa msomaji huathiriwa na tajiriba ambao ni Louise Rosenblatt,Wolfgang Iser na Hans Robert Jauss,kundi la pili ni wale wanaochukulia kwamba maana ya msomaji katika nadharia hii hutokana na saikolojia yake,wananadharia wa kundi hili ni pamoja na Norman Holland na David Bleich. Na kundi la mwisho ni wale wananadharia wanaochukulia kuwa mwitiko wa msomaji huathiriwa na masuala ya kijamii na kiutamaduni yanayomzunguka msomaji,mwananadharia wa kundi hili ni Stanley Fish.
NGUZO MAMA ni tamthiliya inayochambua matatizo yanayowakabili akina mama katika juhudi zao za kuendesha harakati za kujikomboa. Katika tamthiliya hii tutawazungumzia wahusika mbalimbali tukiwahusisha na jinsi wanavyoweza kuonekana kwa mitazamo tofautitofauti kwa msomaji tukiwahusisha na wakati,muktadha na suala la elimu ya msomaji huyo husika.
Kiwakati tunaweza kuigawa tamthiliya hii katika vipindi vikuu viwili. Vipindi hivyo ni kipindi kabla ya mwaka 1975 na kipindi baada ya mwaka huo. Mwaka 1975 ulitangazwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni  mwaka wa wanawake duniani. Tangu wakati huo juhudi zimekuwa zikifanywa kuwakomboa wanawake kutokana na ukandamizwaji na udhalilishwaji mpaka sasa,katika mwaka huo mkutano wa kwanza unaohusu masuala ya wanawake uliitishwa na Umoja wa Mataifa na ulifanyika katika Jiji la Mexico,ukafautiwa na mikutano mingine kama ifuatavyo,ule wa Copenhagen(1980),wa Nairobi (1985) na ule unaotajwa zaidi wa Beijing(1995) pamoja na mingine iliyoendelea kufanyika Beijing kwa miaka iliyofuata hata hivi karibuni kwa ajili ya kuzungumzia na kuwekea mipango masuala mbalimbali ya kumwinua mwanamke katika nyanja zote za maisha. Ni dhahiri kwamba kabla ya mwaka 1975 juhudi za dhati za kumkomboa na kumwinua mwanamke hazikufanyika kikamilifu.
Kwa kuzingatia nadharia hii ya mwitiko wa msomaji na tukirejelea wakati kama tulivyougawa hapo juu,kabla ya mwaka 1975 mtu ambaye angesoma tamthilya hii ya NGUZO MAMA angemchukulia mhusika Bi Nane kama mwanamke mwenye kiburi na  jeuri kubwa kwa sababu alikuwa akiwahamasisha wanawake wenzake kupigania haki zao kwa kuwapa ushauri wa aina mbalimbali kisomi na kuwashauri watumie maarifa na pia na kuwashirikisha wnajamii wote. Msomaji wa kipindi hicho cha kabla ya mwaka 1975 angeweza kumtazama mhusika huyu kwamba ni mwenye kiburi na jeuri kwa sababu masuala ya haki za wanawake na harakati za kudai usawa wa kijinsia hayakuwa yakizungumzwa kwa uwazi kwa kiasi kikubwa na hapakuwa na wanawake waliokuwa ujasiri mkubwa wa kusimama na kuzungumzia masuala ya haki zao na akasikilizwa akaeleweka vizuri kwa wote.
Kwa mfano katika ukurasa wa 73,kuna majibizano yafuatayo;
BI NANE; Jamani tutumie maarifa pia. Tutumie kamba, tutumie zana.
BI NNE; Inuaaa! (wanainua)
BI NANE; Tushirikishe wanaume pia. NGUZO MAMA ina faida kwa wote.
BI NNE; Inuaaa! (Wanainua)
BI NANE; Tuite na watoto wote-wao taifa la kesho.
BI NNE; Inuaaa! Inuaaa!( Wanainua)
Ila wakati wa baada ya mwaka 1975, msomaji huyohuyo asingeweza kushangaa au kuwa na mtazamo hasi dhidi ya mhusika Bi Nane kwani masuala ya haki za wanawake na usawa wa kijinsia yalikuwa yameshawekwa wazi na kuanza kuhimizwa zaidi mahala pengi.
Kimuktadha tunaweza kuigawa tamthiliya hii katika miktadha ifuatayo; muktadha wa kidini na muktadha wa kiutamaduni.
Katika muktadha wa kidini,tunaona msomaji ambaye anazingatia sana muktadha wa kidini mathalani katika dini ya Kikristo ambapo hata Biblia inasema  katika Waefeso (5:2) “Enyi wake watiini waume zenu kama kumtii bwana wetu” au Wakolosai (3:18) inavyosema “ Ninyi wake watiini waume zenu kama impendezanyo Bwana,atamwona mhusika Bi Nane kama anayeenda kinyume na neon la Mungu. Hivyo ataweza kumpuuza tu na anaweza kuhitimisha kwamba ndiyo maana hata NGUZO MAMA haikuweza kuinuka mpaka mwisho pamoja na juhudi zao zote, Lakini mtu ambaye hazingatii dini ataona juhudi za mhusika Bi Nane na wenzie ni jitihada za kujiletea ukombozi/maendeleo yanayohitajika lakini hazikufanikiwa kwa sababu walikosa msimamo na ushirikiano wao kwa wao na hata kutoka katika jamii yote.
Katika muktadha wa kiutamaduni, msomaji anayeamini katika mila na desturi za jadi kama ile ya kwamba  mwanamke hapaswi kurithi/kumiliki mali akiwasoma wahusika Kiando na Makange ataona walichokifanya kwa Bi Saba ni sahihi kabisa yaani kumnyang’anya Bi Saba watoto na  mali zote zilizoachwa na marehemu mumewe bila msaada wowte pamoja na kuwauliza kwa sauti hakuna aliyejitokeza kumsaidia. Lakini msomaji ambaye hazingatii mila kama hizo(za jadi) ataona kwamba wahusika haohao Kiando na Makange wanastahili kupingwa kwa nguvu zote na hata kuchukuliwa hatua za kisheria kwani mambo kama hayo hayakubaliki katika wakati kama huu.
Kwa upande wa elimu ya msomaji,Fish kama alivyonukuliwa na Anderson(2012:    )anasema msomaji si mtu yeyote tu bali ni yule mwenye umilisi wa lugha katika nyanja za fasihi na isimu. (Tafsiri yetu).
Msomaji ambaye ni msomi aliyepevuka kimawazo akisoma tamthiliya ya NGUZO MAMA na kukutana na mhusika kama Bi Nne ambaye alikuwa kiongozi katika Baraza la Wanawake ataona kabsa kwamba mhusika huyu anakiuka maadili ya uongozi bora kutokana na tabia zake za kujiona kama yeye ndiye mwenye kauli zaidi na pia hasikilizi ushauri wa wengine,wakati msomaji huyohuyo kama ni msomi ambaye hajapevuka huweza pia kumuona mhusika huyo Bi Nne hakuwa na shida katika uongozi wake na ndivyo inavyopaswa kuwa katika uogozi,inapaswa viongozi kujiamulia mambo bila kuwashirikisha wanaowasimamia.
Pia msomaji ambaye ni msomi aliyepevuka kimawazo akimtazama mhusika Bi Nane ataona kuwa alikuwa sahihi katika mambo mengi aliyoyafanya kama kuwashauri wenzake kisomi na hivyo anapaswa kuungwa mkono katika jitihada zake za kutaka kuwaunganisha wanawake wenzake na kupigania ukombozi na msomaji huyo atagundua ni kwanini nguzo mama haikuinuka hadi mwisho,lakini msomaji  msomi ambaye hajapevuka ataona kuwa kazi hiyo ni simulio fulani tu na pengine asilichukulie kama lina maana yoyote katika jamii.
Kwa kuhitimisha,tunaweza kusema kwamba kazi ya fasihi inaweza kuwa moja na kuwa na wahusika walewale lakini tafsiri ya wasomaji juu yao ikatofautiana na msomaji mmoja na mwingine kutokana na mambo kama vile wakati/historia,muktadha,elimu,falsafa na mtazao wa msomaji huyo.


MAREJELEO
Anderson. M. (2012); Reader- Response Theories and Life Narratives, Integrated Studies Project, Athabasca University,
Lobo  .A. G. (2015); Reader-Response; A Path Towards Wolfgang Iser, Costa Rica, Universidad Nacional.
Senkoro F.E.M.K. (1982) Fasihi,Dar es Salaam,Press and Publicity
Wafula R. M. na K.  Njogu (2007); Nadharia za Uhakiki wa Fasihi,Nairobi,Sai Industries LTD.

Familia ya Maamkio Mapanda(1967); Biblia Takatifu,Iringa, Parokia ya Usokani

1 comment:

  1. Emperor Casino Review and Ratings | Shootercasino
    Emperor Casino febcasino has many 제왕카지노 exciting bonuses, including 바카라 사이트 hundreds of free spins and a top-quality customer service for its players. Rating: 4 · ‎Review by Shootercasino

    ReplyDelete