UTANGULIZI
Katika insha hii tutahakiki tamthiliya ya NGUZO MAMA iliyoandikwa na Penina
Mhando mwaka 1982 kwa kutumia nadharia ya mwitiko wa msomaji. Katika kulijibu
swali hili tutaanza kwa kufafanua istilahi muhimu zijitokezazo katika swali
yaani wahusika wa kazi ya fasihi,dhana za wakati,muktadha na elimu. Kisha
tutaifafanua nadharia ya mwitiko wa msomaji na kuwajadili wahusika
wanaojitokeza katika tamthiliya ya NGUZO
MAMA kwa kutumia nadharia tajwa kwa kuzingatia vipengele vya wakati,muktadha
na elimu ya msomaji.
Senkoro
(1982:08) anasema, wahusika wa kazi ya fasihi ni watu ama viumbe
waliokusudiwa wawakilishe tabia za watu katika kazi ya fasihi.
Pia Msokile(1992: ) anasema wahusika ni watu au viumbe
katika kazi ya fasihi waliokusudiwa kuwakilisha tabia za watu katika maisha
halisi. Wahusika katika hadithi za mapokeo na hadithi fupi kwa kawaida huwa ni
wanyama, wadudu,mashetani na mizungu.
Wamitila(2003:123)
anaeleza kuwa mhusika ni kiumbe anayepatikana katika kazi ya kifasihi na ambaye
anafanana na binadamu kwa kiasi fulani. Wasifu wa mhusika unategemea mkabala
uliopo.kazi zinaegemezwa katika mitazamo ya kihalisia na zinamsawiri mhusika
kwa namna inayokaribiana sana na binadamu katika ulimwengu wa kawaida.
Hivyo tunaweza kusema kwamba,wahusika ni viumbe hai
na visivyo hai ambavyo hutumiwa katika kazi za kifasihi ili kuwakilisha tabia
halisi za binadamu.
TUKI(2013:630)
wanaeleza kwamba wakati ni muda.majira,mwia,wakaa au wasaa. Katika kazi
hiidhana ya wakati itachukuliwa kama kipindi fulani cha utokeaji wa tukio.
Msokile(1992: ) anafasili muktadha
kuwa ni mazingira au hali inayoathiri maana ya neno,sentensi au kazi ya
sanaa.anaongeza kuwa kazi yoyote lazima iathiriwe na muktadha. Aidha dhana muktadha
katika kazi hii litatumika kama mazingira au hali ya utokeaji wa jambo kama
vile kisiasa, kijamii na kiuchumi.
TUKI(2013:17)
wanasema elimu ni mfumo wa mafunzo yanayopatikana shuleni,vyuoni au maishani,
ni taaluma. Katika kazi hii istilahi elimu itatumiwa kumaanisha uwezo au upeo
wa fikra za mtu kutokana na taaluma
yake.
Nadharia
ya mwitiko wa msomaji
Huu ni mkabala wa kifasihi ambao matilaba yake ni
kuwaelezea wasomaji au wasikilizaji wa kazi ya fasihi namna wanavyoweza kuisoma
na kuielewa kazi ya fasihi kutokana na elimu yao,mazingira na wakati.
Wafula
na Njogu (2007:85) wanasema ni nadharia inayosughulikia upokeaji
wa matini za fasihi kuhusu ulimbwende na mitizamo ya kisaikolojia. Kimapokeo
msomaji huwa na mawazo juu ya matini anayopitia. Kutokana na tajiriba ya
usomaji,msomaji hupata hisi maalumu. Utunzi na upokeaji wa sanaa hushirikishwa
sana na hisi kwa mujibu wa imani na nadharia za kilimbwende. Hizi ndizo humpa mwanasanaa
msukumo wa kutunga. Vilevile,msomaji anatazamiwa kupokea kazi ya fasihi kwa
kuzingatia mielekeo yake binafsi.
Lobo(2015:13)
anasema nadharia ya mwitiko wa msomaji inafafanua mahusiano yaliyopo baina ya
wasomaji na matini ili kuonesha maana ya kazi ya fasihi.(tafsiri yetu).
Kwa mtazamo wetu,huu ni mkabala wa kifasihi ambao
matilaba yake ni kumwelezea msomaji au msikilizaji wa kazi ya fasihi na namna
wanavyoweza kuisoma na kuielewa kazi ya fasihi na kuipa maana kutokana na
elimu,historia,mazingira yao na hata msimamo na mtazamo wao katika maisha.
Wafula
na Njogu(2007:85) wanasema waasisi na watetezi wakuu wa
nadharia ya mwitiko wa msomaji ni Stanley Fish(1980), Jane Tompkins(1980) na
Wolfgang Iser(1974,1978).
Anderson
(2012:06-07) aliwagawa wananadharia wanaosimamia
nadharia hii katika makundi matatu. Kundi la kwanza ni wale wanaoona kwamba
mwitiko wa msomaji huathiriwa na tajiriba ambao ni Louise Rosenblatt,Wolfgang
Iser na Hans Robert Jauss,kundi la pili ni wale wanaochukulia kwamba maana ya
msomaji katika nadharia hii hutokana na saikolojia yake,wananadharia wa kundi
hili ni pamoja na Norman Holland na David Bleich. Na kundi la mwisho ni wale
wananadharia wanaochukulia kuwa mwitiko wa msomaji huathiriwa na masuala ya
kijamii na kiutamaduni yanayomzunguka msomaji,mwananadharia wa kundi hili ni
Stanley Fish.
NGUZO
MAMA
ni tamthiliya inayochambua matatizo yanayowakabili akina mama katika juhudi zao
za kuendesha harakati za kujikomboa. Katika tamthiliya hii tutawazungumzia
wahusika mbalimbali tukiwahusisha na jinsi wanavyoweza kuonekana kwa mitazamo
tofautitofauti kwa msomaji tukiwahusisha na wakati,muktadha na suala la elimu
ya msomaji huyo husika.
Kiwakati
tunaweza kuigawa tamthiliya hii katika vipindi vikuu viwili. Vipindi hivyo ni
kipindi kabla ya mwaka 1975 na kipindi baada ya mwaka huo. Mwaka 1975
ulitangazwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni
mwaka wa wanawake duniani. Tangu wakati huo juhudi zimekuwa zikifanywa
kuwakomboa wanawake kutokana na ukandamizwaji na udhalilishwaji mpaka
sasa,katika mwaka huo mkutano wa kwanza unaohusu masuala ya wanawake uliitishwa
na Umoja wa Mataifa na ulifanyika katika Jiji la Mexico,ukafautiwa na mikutano
mingine kama ifuatavyo,ule wa Copenhagen(1980),wa Nairobi (1985) na ule
unaotajwa zaidi wa Beijing(1995) pamoja na mingine iliyoendelea kufanyika
Beijing kwa miaka iliyofuata hata hivi karibuni kwa ajili ya kuzungumzia na
kuwekea mipango masuala mbalimbali ya kumwinua mwanamke katika nyanja zote za
maisha. Ni dhahiri kwamba kabla ya mwaka 1975 juhudi za dhati za kumkomboa na
kumwinua mwanamke hazikufanyika kikamilifu.
Kwa kuzingatia nadharia hii ya mwitiko wa msomaji na
tukirejelea wakati kama tulivyougawa hapo juu,kabla ya mwaka 1975 mtu ambaye
angesoma tamthilya hii ya NGUZO MAMA angemchukulia
mhusika Bi Nane kama mwanamke mwenye
kiburi na jeuri kubwa kwa sababu alikuwa
akiwahamasisha wanawake wenzake kupigania haki zao kwa kuwapa ushauri wa aina
mbalimbali kisomi na kuwashauri watumie maarifa na pia na kuwashirikisha
wnajamii wote. Msomaji wa kipindi hicho cha kabla ya mwaka 1975 angeweza
kumtazama mhusika huyu kwamba ni mwenye kiburi na jeuri kwa sababu masuala ya
haki za wanawake na harakati za kudai usawa wa kijinsia hayakuwa yakizungumzwa
kwa uwazi kwa kiasi kikubwa na hapakuwa na wanawake waliokuwa ujasiri mkubwa wa
kusimama na kuzungumzia masuala ya haki zao na akasikilizwa akaeleweka vizuri kwa
wote.
Kwa
mfano katika ukurasa wa 73,kuna majibizano yafuatayo;
BI
NANE;
Jamani tutumie maarifa pia. Tutumie kamba, tutumie zana.
BI
NNE;
Inuaaa! (wanainua)
BI
NANE; Tushirikishe
wanaume pia. NGUZO MAMA ina faida kwa wote.
BI
NNE;
Inuaaa! (Wanainua)
BI
NANE;
Tuite na watoto wote-wao taifa la kesho.
BI
NNE;
Inuaaa! Inuaaa!( Wanainua)
Ila wakati wa baada ya mwaka 1975, msomaji huyohuyo
asingeweza kushangaa au kuwa na mtazamo hasi dhidi ya mhusika Bi Nane kwani masuala ya haki za
wanawake na usawa wa kijinsia yalikuwa yameshawekwa wazi na kuanza kuhimizwa
zaidi mahala pengi.
Kimuktadha
tunaweza kuigawa tamthiliya hii katika miktadha ifuatayo; muktadha wa kidini na
muktadha wa kiutamaduni.
Katika muktadha
wa kidini,tunaona msomaji ambaye anazingatia sana muktadha wa kidini
mathalani katika dini ya Kikristo ambapo hata Biblia inasema katika Waefeso (5:2) “Enyi wake watiini waume
zenu kama kumtii bwana wetu” au Wakolosai (3:18) inavyosema “ Ninyi wake
watiini waume zenu kama impendezanyo Bwana,atamwona mhusika Bi Nane kama
anayeenda kinyume na neon la Mungu. Hivyo ataweza kumpuuza tu na anaweza
kuhitimisha kwamba ndiyo maana hata NGUZO MAMA haikuweza kuinuka mpaka mwisho
pamoja na juhudi zao zote, Lakini mtu ambaye hazingatii dini ataona juhudi za
mhusika Bi Nane na wenzie ni jitihada za kujiletea ukombozi/maendeleo
yanayohitajika lakini hazikufanikiwa kwa sababu walikosa msimamo na ushirikiano
wao kwa wao na hata kutoka katika jamii yote.
Katika muktadha
wa kiutamaduni, msomaji anayeamini katika mila na desturi za jadi kama ile
ya kwamba mwanamke hapaswi
kurithi/kumiliki mali akiwasoma wahusika Kiando
na Makange ataona walichokifanya kwa
Bi Saba ni sahihi kabisa yaani
kumnyang’anya Bi Saba watoto na mali zote zilizoachwa na marehemu mumewe bila
msaada wowte pamoja na kuwauliza kwa sauti hakuna aliyejitokeza kumsaidia. Lakini
msomaji ambaye hazingatii mila kama hizo(za jadi) ataona kwamba wahusika haohao
Kiando na Makange wanastahili kupingwa kwa nguvu zote na hata kuchukuliwa
hatua za kisheria kwani mambo kama hayo hayakubaliki katika wakati kama huu.
Kwa upande wa elimu
ya msomaji,Fish kama alivyonukuliwa na Anderson(2012: )anasema msomaji si mtu yeyote tu bali
ni yule mwenye umilisi wa lugha katika nyanja za fasihi na isimu. (Tafsiri
yetu).
Msomaji ambaye ni msomi aliyepevuka kimawazo akisoma
tamthiliya ya NGUZO MAMA na kukutana na mhusika kama Bi Nne ambaye alikuwa kiongozi katika Baraza la Wanawake ataona
kabsa kwamba mhusika huyu anakiuka maadili ya uongozi bora kutokana na tabia
zake za kujiona kama yeye ndiye mwenye kauli zaidi na pia hasikilizi ushauri wa
wengine,wakati msomaji huyohuyo kama ni msomi ambaye hajapevuka huweza pia
kumuona mhusika huyo Bi Nne hakuwa
na shida katika uongozi wake na ndivyo inavyopaswa kuwa katika uogozi,inapaswa
viongozi kujiamulia mambo bila kuwashirikisha wanaowasimamia.
Pia msomaji ambaye ni msomi aliyepevuka kimawazo
akimtazama mhusika Bi Nane ataona
kuwa alikuwa sahihi katika mambo mengi aliyoyafanya kama kuwashauri wenzake
kisomi na hivyo anapaswa kuungwa mkono katika jitihada zake za kutaka
kuwaunganisha wanawake wenzake na kupigania ukombozi na msomaji huyo atagundua
ni kwanini nguzo mama haikuinuka hadi mwisho,lakini msomaji msomi ambaye hajapevuka ataona kuwa kazi hiyo
ni simulio fulani tu na pengine asilichukulie kama lina maana yoyote katika
jamii.
Kwa kuhitimisha,tunaweza kusema kwamba kazi ya
fasihi inaweza kuwa moja na kuwa na wahusika walewale lakini tafsiri ya wasomaji
juu yao ikatofautiana na msomaji mmoja na mwingine kutokana na mambo kama vile
wakati/historia,muktadha,elimu,falsafa na mtazao wa msomaji huyo.
MAREJELEO
Anderson. M. (2012); Reader- Response Theories and
Life Narratives, Integrated Studies Project, Athabasca University,
Lobo .A. G.
(2015); Reader-Response; A Path Towards Wolfgang Iser, Costa Rica, Universidad
Nacional.
Senkoro F.E.M.K. (1982) Fasihi,Dar es Salaam,Press
and Publicity
Wafula R. M. na K.
Njogu (2007); Nadharia za Uhakiki wa Fasihi,Nairobi,Sai Industries LTD.
Familia ya Maamkio Mapanda(1967); Biblia
Takatifu,Iringa, Parokia ya Usokani